Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo mchana, katika kikao na Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Magavana wa mikoa, alisisitiza kuwa magavana ni viongozi muhimu katika mikoa yao, na akaelezea kuwa mazingira ya jumla ya nchi yako sawa kwa ajili ya kutoa huduma bora na fursa nyingi zipo. Katika kutoa baadhi ya maelekezo, alisema: Miongoni mwa mambo muhimu zaidi ni suala la wananchi; lazima muende kwao, muhudhurie katika mikusanyiko yao, msikilize kwa subira maneno yao hata kama ni makali, na pia mtoeni maelezo muhimu yanayohitajika.
Akiashiria kwamba nchi imejaa fursa nyingi na haina changamoto kubwa kama vile vita, magonjwa makubwa kama Corona, matatizo makubwa ya kiusalama, au migongano ya kisiasa na mirengo ya kiitikadi iliyojaa, alibainisha kuwa: Pamoja na hayo yote, nchi ina rasilimali kubwa ya nguvu kazi ya vijana walioelimika na wenye ufanisi, ambao iwapo kila taasisi itawatambua na kutumia uwezo wao, mafanikio makubwa na yanayoonekana yataweza kupatikana.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia alitaja kuwa miongoni mwa fursa nyingine muhimu ni "ushiriki wa Iran katika taasisi muhimu za kikanda na za kimataifa" kama vile "Shanghai na BRICS", pamoja na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani mikononi mwa waziri anayefahamu vizuri maeneo mbalimbali ya nchi.
Akiwashauri kuhusu uteuzi wa viongozi wa mikoa, alisema: Chagueni viongozi walio na moyo wa kutoa huduma na waliosafi kimaadili kwa ajili ya kuendesha mambo. Ikiwa viongozi wenye sifa hizi watachaguliwa, basi hakutakuwa na fursa yoyote ya kazi na maendeleo inayopotea.
Ayatollah Khamenei alitaja "kupambana na ufisadi" kuwa ni moja ya majukumu ya msingi ya viongozi wakuu, na akasisitiza kwamba: Sharti la msingi na la kwanza katika kupambana na ufisadi ni "viongozi na familia zao kuwa mbali na vyanzo vya ufisadi".
Aliongezea kusema kuwa: Madhara na hasara ya kiongozi kuingia kwenye ufisadi, kutokana na nafasi yake nyeti, ni mara dufu, na adhabu yake mbele ya Mwenyezi Mungu pia ni mara mbili zaidi. Hata hivyo, kama nilivyosisitiza katika ujumbe wangu mrefu na muhimu wa miaka iliyopita, ufisadi ni kama joka lenye vichwa saba ambalo haliwezi kuangamizwa kwa urahisi. Mapambano dhidi ya ufisadi lazima yaendelee.
Katika nasaha nyingine, alisisitiza tena kuwa; viongozi na magavana wawe karibu na wananchi, wajichanganye nao, na wawasikilize kwa subira hata maneno yao yatakuwa makali, kisha akaongeza kusema: Jambo hili litaleta mapenzi kati yenu na wananchi na mtapata msaada wao katika nyakati muhimu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia aliwausia magavana kuwa wacha Mungu, waepuke mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, wajikite katika kufuata mila za kidini, wajitahidi kutekeleza kaulimbiu ya mwaka, na wapambane kwa dhati na kwa pamoja dhidi ya bidhaa za magendo.
Maoni yako